MAFUNZO YA HIMOFILIA KWA WATAALAMU WA MAABARA HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA YA TEMEKE YAHITIMISHWA KWA MAFANIKIO MAKUBWA

Posted on: June 20th, 2025

Mafunzo ya siku mbili kwa wataalamu wa maabara katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Temeke juu ya magonjwa ya damu hasa ugonjwa wa Himofilia ambayo yametolewa chini Chama cha Himofilia Tanzania kwa kushirikiana na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili yamehitimishwa rasmi tarehe 20 Juni, 2025 kwa mafanikio makubwa

Mafunzo hayo yalilenga kutoa uelewa kwa wataalamu wa Maabara kuhusu ugonjwa wa Himofilia ambao unahusisha tatizo la damu kuganda ambapo wagonjwa wenye tatizo hilo hupata tatizo la kutokwa na damu muda mrefu bila kukata mara wanapopata jeraha au changamoto nyingine

Akizungumzia namna mafunzo hayo yalivyofanyika na matokeo yake Meneja mradi huo Theophil Kayombo amesema mafunzo hayo yamefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Temeke ambapo kwa siku mbili walizofanya mafunzo ya nadharia na vitendo wamefanikiwa kutambua wagonjwa wapya wawili ambao wamepimwa na kukutwa na changamoto hiyo

“Utambuzi wa Ugonjwa wa Himofilia unataka utaalamu wa juu zaidi hivyo tumeleta wataalamu wenye uzoefu kutoka Tanzania na nje ya nchi ili kuwajengea uwezo wataalamu wengine, tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa kwasababu Tanzania nzima tulikuwa na wagonjwa waliogundulika wa Himofilia 502 tu ambapo kwa siku mbili tumefanikiwa kupata wagonjwa wapya wawili hapa Temeke”, Alisema Theopil Kayombo – Meneja Mradi wa Himofilia Tanzania


Kwa upande wake Meneja wa Maabara Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Temeke Venance Mlowe amesema mafunzo hayo yatawasaidia wataalamu wa maabara kufanya uchunguzi na kuwatambua wagonjwa wenye changamto hiyo kiurahisi, pia amewata hofu wananchi kuwa huduma za maabara Hospitali ya Temeke zimeboreshwa na sasa huduma zote za uchunguzi wa magonjwa zinaweza kufanyika kikamilifu