WATUMISHI WAKALA WA VIPIMO WAISHUKURU HOSPITALI YA TEMEKE KWA KUWAPELEKEA CHANJO YA HOMA YA INI

Posted on: September 8th, 2024

Dar es Salaam, 09 Septemba, 2024

Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke imefanikiwa kutoa chanjo ya Homa ya ini kwa watumishi 40 wa Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA) ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za serikali kupitia Wizara ya Afya katika kuhakikisha wananchi wanakuwa salama dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa homa ya ini kwa kupata chanjo.

Akizungumzia zoezi hilo Afisa Afya wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke Juhudi Nyambuka amesema watumishi wa (WMA) wamekuwa na mwamko mkubwa wa kujitokeza kupata chanjo ndiomana kama Hospitali ya Temeke wamemua kufika katika ofisi za wakala huo ili kuwapa huduma hiyo na kwa siku ya leo watumishi 40 wamepatiwa chanjo.

Kutokana na taarifa za shirika la kupambana na magonjwa Marekani (CDC), takriban watu milion 296 wana maambukizi ya virusi vya hepatitis B vinavyosababisha homa ya Ini. Kati ya hawa, kati ya asilimia 15-25 wapo hatarini kupoteza maisha kutokana na homa ya ini , uharibufu wa ini, saratani ya ini au changamoto nyingine zinazochangiwa na maambukizi ya virusi hivi.

Kila mwaka takribani watu 820,000 hupoteza maisha yao kutokana na virusi vya Hepatitis B ambavyo huambukizwa kupitia damu. Ugonjwa huu unaweza kuzuiwa kwa kupata chanjo tatu ambazo zitamlinda mchanjwaji kwa maisha yake yote.

Nao baadhi ya watumishi wa Wakala wa Vipimo (WMA) wameishukuru Hospitali ya Temeke kupitia mganga mfawidhi wa Hospitali hiyo Dkt. Joseph Kimaro kwa kuwapelekea huduma ya chanjo mpaka ofisini kwao ambapo pia wametoa wito kwa wananchi na watumishi wengine wa serikali katika taasisi mbalimbali kuendelea kuchangamkia fursa ya kupata chanjo ili wajihakikishie usalama wao na wanaowazunguka dhidi ya ugonjwa wa homa ya ini.