Kliniki ya Afya ya Akili na magonjwa ya akili iliopo Temeke Hospitali Yasherekea Siku ya Afya ya Akili Duniani kwa kufanya usafi na Wadau mbalimbali

Posted on: October 10th, 2023
Dar es salaam, Tarehe 10 Oktoba 2023* 

 Kila tarehe kumi ya mwezi wa kumi, Tanzania inaadhimisha Siku ya Afya ya Akili Duniani, na hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke imeonyesha uongozi katika jamii kwa kuadhimisha siku hii muhimu. Kliniki ya magonjwa na afya ya akili katika hospitali hiyo, inayohudumia watu 350 kila mwezi wenye changamoto za afya ya akili, imeonyesha jukumu lake kwa kufanya usafi wa mazingira katika maeneo ya nje ya hospitali. 

 Usafi huo wa mazingira uliowashirikisha wadau wa afya ya akili na mazingira, pamoja na utoaji wa elimu juu ya afya ya akili, maambukizi, na jinsi ya kujikinga na ugonjwa wa kifua kikuu (TB), ulikuwa mwangaza katika kushughulikia changamoto hizi za kiafya.

 Daktari Bingwa wa Magonjwa na Afya ya Akili katika hospitali hiyo, Dkt. Francis, amesema, "Tumelenga kutoa elimu ya afya ya akili kwa watu elfu moja, ikiwa ni pamoja na waraibu wa dawa za kulevya, wagonjwa wa afya ya akili, na wagonjwa waliopo opd. Wagonjwa wa afya ya akili wanapona vizuri kabisa na wanapaswa kutambua kwamba wanaweza kupata msaada katika vituo vya afya."

 Kwa upande wake, Afisa wa Afya Mazingira Bi. Juhudi Nyambuka ameelezea kwamba usafi huo ulilenga pia kujiandaa na mvua za El Nino zinazotarajiwa kuanza. 

"Kupitia usafishaji na uchimbuaji mitaro, tunalenga kusaidia hospitali yetu na jamii inayozunguka maeneo ya hospitali. Tunatoa wito kwa wadau wote kuungana nasi katika kudumisha usafi na afya ya jamii yetu."

Bw. Ally Bofu, mdau wa afya ya akili ambae pia ni mlemavu wa viungo, ametoa ushuhuda mzito kuhusu ushiriki wake katika tukio hilo. Amesema, 

"Siku ya leo ni siku ya watu wenye ulemavu wa akili, lakini kama mlemavu mwingine, nimeguswa kusaidia jamii yetu. Tusiwe nyuma; hata kama una changamoto, unaweza kuchangia katika kuboresha jamii. Jitume na tujichanganye na wengine walio wazima; kila mtu ana thamani na mchango wake katika jamii."

 Wakati huo huo, mmoja wa waliopata matibabu na sasa amepata ahueni, Bw. Said, aliwashauri wengine waliopatwa na changamoto za afya ya akili kufika katika vituo vya afya kupata matibabu. Amesema, 

"Madaktari wanajua namna ya kutibu watu wenye changamoto ya afya ya akili. Usiogope kutafuta msaada; kupata matibabu ni hatua ya kwanza kuelekea kupona na kuwa sehemu ya jamii yenye afya na furaha."

 Kwa jumla, ushiriki wa kliniki ya magonjwa ya afya ya akili katika maadhimisho haya umekuwa mwangaza wa matumaini na elimu kwa jamii ya Watanzania, ukihakikisha kwamba hakuna mtu anayeachwa nyuma katika safari ya kuboresha afya ya akili na kujenga jamii yenye uelewa na huruma."