HUDUMA ZA AFYA HOSPITALI YA TEMEKE ZAWAKOSHA WABUNGE KUTOKA AFRIKA NA ASIA WALIOFIKA KUJIONEA HUDUMA ZINAVYOTOLEWA

Posted on: February 25th, 2025


Waheshimiwa hao kutoka Chama cha Kibunge kinachoundwa na nchi za Asia na Afrika leo wamefanya ziara katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Temeke kama sehemu ya kujifunza na kujionea namna huduma mbalimbali zinavyotolewa hasa huduma za mama na mtoto

Katika ziara hiyo waheshiwa wabunge wameongozwa na Mhe. Pemmy Majodina ambaye ni Mbunge kutoka bunge la Afrika ya Kusini Pamoja na Mhe. Sebastiani Kafupi ambaye ni mbunge wa Mpanda Mjini ambao wamekoshwa na namna huduma bora zinavyotolewa Hospitali ya Temeke na uwekezaji mkubwa wa serikali katika vifaa tiba vilivyochangia kipunguza vifo kwa wajawazito na kuboresha huduma nyingine ikiwemo za CT Scan na X-ray


Akizungumza katika Ziara hiyo Mbunge wa Mpanda Mjini Mhe. Sebastian Kafupi amesema lengo la ziara hiyo Hospitali ya Temeke ni kujionea kazi kubwa iliyofanywa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Hospitali ya Temeke ambapo wote wameridhishwa na huduma zinavyotolewa na jinsi ambavyo serikali imewekeza katika kuhakikisha huduma bora za Afya zinatolewa

Kwa upande wake Mganga Mfawidhi Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Temeke Dkt. Joseph Kimaro amesema ni furaha kubwa kwa Hospitali kuona wabunge kutoka mataifa Mbalimbali wanafika Hospitali ya Temeke kuona huduma zinavyotolewa na kupongeza huduma hizo ambapo amesema huu ni uthibitisho kwamba serikali imewekeza katika Hospitali ya Temeke na matokeo yanaonekana kila siku


Nae Mwenyekiti ya Bodi ya Ushauri ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Temeke Dkt. Deus Buma amesema ujio wa wageni hao ni ishara kwamba Huduma za Afya Hospitali ya Temeke zimeboreshwa na zimekuwa kivutio kwa wengi kuja kujionea na kujifunza ambapo yote yamechangiwa na uwekezaji mkubwa wa serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika huduma za Afya nchin.