HOSPITALI ZA RUFAA ZA MIKOA ZAPONGEZWA KWA KUBORESHA HUDUMA KWA WANANCHI

Posted on: September 18th, 2024

Dar es Salaam, 19 Septemba, 2024


Serikali imesema ubora wa huduma za Afya zinazotolewa na Serikali katika Hospitali za Rufaa za Mikoa nchini umekuwa na mchango mkubwa katika kupunguza gharama za matibabu kwa wananchi

Hayo yamesemwa Septemba 18, 2024 na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Juma Homera wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha Waganga Wafawidhi, Wauguzi Wafawidhi, Makatibu wa Hospitali na Waratibu wa Ubora wa Huduma(QI) wa Hospitali za Rufaa za Mikoa ya Tanzania bara

Mhe. Homera amesema Uboreshaji wa vifaa, majengo na utaalamu katika Hospitali za Rufaa za Mikoa umewezesha wananch kupata matibabu sahihi kwa wakati, kuepuka gharama za matibabu.

Amesema hospitali hizo zimepunguza rufaa za wagonjwa kwa kuwa huduma za kibingwa zipo kwenye mikoa na hivyo kuepuka gharama za ziada zilizo sababishwa na ucheleweshaji wa huduma.


"Wananchi wengi wameweza kupata huduma za afya za kibingwa ndani ya mikoa yao bila kulazimika kusafiri umbali mrefu kwenda hospitali za Taifa au nje ya nchi, hii imepunguza gharama kubwa kwa Wananchi" Amesema Mhe. Homera.

Pia Mhe. Homera amewapongeza Waganga Wafawidhi kwa usimamizi mzuri ambao umewezesha kupungua kwa malalamiko kwa wananchi ambapo ametoa wito kwa Waganga wafawidhi kuhakikisha kupitia vitengo vya habari
vilivyopo kutangaza kazi zilizofanywa na Serikali ili wananchi wajue huduma zilivyoboreshwa na zinazotolewa katika hospitali hizo.

"Tuhakikishe tunalipa stahiki vizuri za watumishi waliopo chini yetu, watumishi wakifanya kazi hakikisheni kama wanahitajika kulipwa mmewalipa na kuwe na ukweli na uwazi katika taasisi zetu kila mtu anatakiwa kuhudumiwa vizuri."


Nae Mkurugenzi Msaidizi anae simamia Huduma za Hospitali kutoka Wizara ya Afya Dkt. Caroline Damian Caroline amesema lengo serikali ya awamu ya sita ni kuhakikisha uwekezaji uliofanywa una tafsiriwa katika huduma za afya zenye ubora kwa wananchi wote wa Tanzania

"Miongoni mwa mikakati tutakayo iweka kwa pamoja na kukubaliana kutokana na kikao hiki ni kuhakikisha tuna simamia utoaji wa motisha
kwa watumishi wa sekta ya afya ili waweze kufanya kazi kwa morali na kutoa huduma bora" Amesema Dkt. Caroline.