HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA TEMEKE KWA USHIRIKIANO NA AMERICAN SOCIETY FOR MICROBIOLOGY (ASM) NA FLEMING FUND YABORESHA HUDUMA ZA MAABARA NA UCHUNGUZI WA VIMELEA

Posted on: March 12th, 2025

Dar es salaam 17 Machi, 2025

Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke, kwa kushirikiana na American Society for Microbiology (ASM) kupitia mradi wa Fleming Fund, imepokea rasmi vifaa vya kisasa vya maabara vitakavyosaidia kuboresha huduma za uchunguzi wa vimelea kwa usahihi na kwa haraka zaidi.

Vifaa hivyo vilikabidhiwa rasmi tarehe 17 Machi 2025 na Bi. Ade Olarewaju, M.S, ambaye ni Afisa Mwandamizi wa ASM na kiongozi wa mradi wa Fleming Fund nchini Tanzania. Miongoni mwa vifaa vilivyokabidhiwa ni Automated Blood Culture Analyzer (Bactec Fx40), Autoclave, pamoja na Incubator, ambavyo vitatumika kuboresha huduma za uchunguzi wa magonjwa, usafi wa vifaa vya tiba, na utoaji wa huduma bora za matibabu.



Akizungumza wakati wa hafla ya kupokea vifaa hivyo kwa niaba ya uongozi wa hospitali, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Hospitali ya Temeke, Dkt. Deus Charles Buma, aliishukuru ASM kwa kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuboresha huduma za afya. Alisisitiza kuwa hospitali itavitumia vifaa hivyo ipasavyo ili kuwahudumia wananchi kwa ufanisi mkubwa, kama ilivyokusudiwa na mradi wa Fleming Fund.




Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Temeke, Dkt. Joseph Kimaro, alieleza kuwa kupokelewa kwa vifaa hivyo ni ishara ya ushirikiano madhubuti kati ya taasisi za kimataifa na Serikali ya Tanzania. Vifaa hivi vitasaidia kupunguza idadi ya siku za kusubiria majibu ya kipimo cha damu (Blood Cultrure ) toka siku 7 hadi chini ya siku 3 ambapo maisha ya wagonjwa wengi wakiwemo watoto wachanga yataokolewa.  Alibainisha kuwa msaada huo unaonesha namna ambavyo jumuiya ya kimataifa inaitambua juhudi zinazofanywa na Serikali ya Tanzania hivyo kuendelea kuiunga mkono katika kuboresha sekta ya afya kwa manufaa ya wananchi.




Katika mazungumzo rasmi baina ya Bi. Ade Olarewaju na uongozi wa Hospitali ya Temeke, pande zote mbili zilielezea dhamira ya kuendeleza ushirikiano huu ili kuhakikisha huduma za afya zinaendelea kuimarika, hususan katika eneo la uchunguzi wa vimelea na usalama wa tiba. Aidha walikubaliana kuangalia maeneo mapya ya ushirikiano ikiwemo kufanya tafiti mbalimbali za kimicrobiologia zinazolenga kuboresha utoaji wa huduma za Afya na matumizi bora ya Antibiotiki.

Vifaa vyote vikiwemo Automated Blood Culture Analyzer (Bactec Fx 40), Autoclave, na Incubator vimeshapokelewa, kufungwa na hatua mbalimbali za mafunzo kwa wataalamu wa Hospoitali zinaendelea tayari kuanza huduma hii muhimu.