DKT KIMARO : MSD IMETUWEZESHA KUTOA HUDUMA ZA USHAFISHAJI DAMU KWA GHARAMA NAFUU ZAIDI

Posted on: December 25th, 2024

Mganga Mfawidhi Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Temeke Dkt. Joseph Kimaro ameyasema hayo mnamo 27/12/2024  ofisini kwake Hospitali ya Temeke alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari kuhusu maendeleo ya mashine za kisasa zilizotolewa na MSD katika utoaji wa huduma za usafishaji damu yaani Dialysis kwa wagonjwa  wenye matatizo ya figo 


Dkt. Kimaro amesema kupitia mashine hizo za kisasa zilizotolewa na MSD kupitia Mkurugenzi wake Mavere Tukai zimesaidia kwa kiasi kikubwa katika kuboresha huduma za usafishaji damu, kuongeza mapato ya Hospitali pamoja na kupunguza gharama za utoaji huduma hiyo kwa wananchi ambapo kwasasa huduma za usafishaji damu kwa wenye matatizo ya figo Hospitali ya Temeke zinatolewa kwa gharama nafuu ya shilingi laki moja na elfu hamsini

Hayo yamejiri kufuatilia ziara iliyofanywa na watumishi kutoka (MSD) waliofika katika Hospitali ya Temeke kujionea huduma za usafishaji damu zinavyoendelea kutolewa na namna mashine za kisasa walizozitoa zimesaidia kuboresha huduma hizo kwa wananchi 


"MSD wamefanya jitihada kubwa kutupatia mashine za kisasa ambazo mfumo wake umetupa uhuru wa kushirikiana na wadau wowote katika uendeshaje wake hasa katika kupata Reagents na hiyo imetusaidia kupunguza gharama za utoaji wa huduma hii kuwa nafuu zaidi katika Hospitali ya Temeke kulinganisha na Hosptali nyingine yoyote ya Dar es salaam na hii imesaidia wananchi kupata huduma bora katika eneo bora, wataalamu wazuri na kwa gharama nafuu", Alisema Dkt. Joseph Kimaro Mganga Mfawidhi Hospitali ya Temeke 

Nae Mkuu wa kitengo cha Usafishaji Damu Hospitali ya Temeke Dkt. Emmanuel Lazaro amesema kufutia kuongezeka kwa idadi ya wagonjwa wanaohitaji huduma hiyo kwasasa, uwepo wa mashine hizo za kisasa umesaidia kukidhi idadi ya wagonjwa pasipo kuweka foleni katika utoaji wa huduma 


Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD) Bw. Mavere Tukai ambaye amezungumza kwa njia ya simu amesema lengo la (MSD) ni kuhakikisha kufikia mwaka 2025 gharama za usafishaji damu zishuke zaidi ili kuwasaidia wananchi ambapo amesema matarajio yao ni kuhakikisha huduma hii inatolewa hata kwa gharama ya chini isiyozidi shilingi laki moja


Aidha, amesema Hospitali ya Temeke sio tu watumiaji wa huduma za (MSD) bali wapo mstari wa mbele katika utoaji wa hduma za usafishaji damu pia katika huduma hizo wamekuwa wadau wakubwa katika msaada wa kitaalamu kutoka kwa wataalamu wake.