DC EDWARD MPOGOLO AZINDUA RASMI BODI YA USHAURI YA HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA YA TEMEKE
Posted on: December 19th, 2024Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Edward Mpogolo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Albert Chalamila tarehe 20 Disemba, 2024 amezindua rasmi Bodi ya Ushauri ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Temeke ambayo imeundwa ili kusimamia na kushauri shughuli zote za uendeshaji wa Hospitali
Akizungumza wakati akizindua bodi hiyo rasmi, Mkuu wa Wilaya ya Ilala ambaye amemuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Albert Chalamila ameitaka bodi hiyo kuhakikisha inafuata misingi ya kuundwa kwake ambapo dhumuni la kuundwa kwa bodi hiyo ni kuhakikisa inakuwa chachu ya maendeleo ya Hospitali kwa kuhakikisha huduma bora zinaendelea kutolewa kwa wananchi
“Dhumuhi la kuundwa kwa bodi hizi ni kumsaidia Mhe, Rais kuhakikisha wananchi wake wanapatiwa huduma bora, ni imani yangu na agizo langu kwamba bodi ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Temeke itakuwa chachu ya maendeleo ya Hospitali na kuleta mabadiliko ya utoaji huduma kwa wananchi”, Alisema Mhe. Edward Mpogolo Mkuu wa wilaya ya Ilala
Pia Mhe. Mpogolo ameipongeza Hospitali ya Temeke kwa jitihada zake za kuwasomesha wataalamu wake wa kada mbalimbali ili kuhakikisha huduma za kibingwa zinazidi kuongezeka Hospitali ya Temeke ambapo amemtaka Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Temeke Dkt. Joseph Kimaro kuhakikisha wataalamu hao wanatumika ipasavyo kutoa huduma bora na kupunguza msongamano wa wananchi katika Hosptali ya Taifa Muhimbili
Akizungumza awali wakati akitoa taarifa fupi ya Hospitali, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Temeke Dkt. Joseph Kimaro amesema Hospitali ya Temeke imejitahidi kutumia mapato yake ya ndani kufanya maendeleo mbalimbali ikiwemo kuongeza huduma ambazo hazikuwepo kama vile vipimo vya CT Scan, Huduma za usafishaji damu na huduma nyingine nyingi zilizoboreshwa
Aidha kwa upande wake Mwenyekiti wa bodi ya ushauri ya Hospitali ya Temeke Dkt. Deus Buma ameshukuru kwa kuteuliwa kwake kuiongoza bodi hiyo kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo ambapo amesema bodi hiyo ya ushauri itashirikiana na menejimenti ya Hospitali katika kuhakikisha inatimiza wajibu wake na kuisaidia Hospitali kutoa huduma bora kwa wananchi