AONDOLEWA UVIMBE KILOGRAM 6.4 TUMBONI ULIOMTESA KWA MIAKA 16

Posted on: October 1st, 2024

Dar es Salaam, 02 Oktoba, 2024 



Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke mnamo tarehe 27 Septemba, 2024 imemfanyia upasuaji Zuwena Khamis Mwedadi mwenye umri wa miaka 51 mkazi wa Dar es salaam aliyekuwa akisumbuliwa na tatizo la uvimbe tumboni uliomtesa kwa miaka 16 tangu alipoanza kusumbuliwa na tatizo hilo mwaka 2008

Upasuaji huo umefanywa na jopo la madaktari watatu wakiongozwa na Dkt. Joseph Kiani akisaidiana na Dkt. Abdalallah Mashombo ambapo upasuaji huo umefanyika kwa muda wa saa (4) na kufanikisha kutoa Kilogramu 6.4 za uvimbe ukiambatana na kizazi






Akizungumzia upasuaji huo Daktari bingwa wa Magonjwa ya akina mama na uzazi Hospitali ya Temeke , Dkt. Joseph Kiani amesema mgonjwa huyo alipokelewa Hospitali ya Temeke na kufanyiwa vipimo mbalimbali ili kufahamu chanzo cha uvimbe huo ikiwemo kipimo cha CT Scan ndipo ilipogundulika ana uvimbe mkubwa lakini haikuonesha wapi uvimbe huo umeanzia kwasababu ulikuwa mkubwa sana


Dkt. Kiani anasema awali walishindwa kuendelea na upasuaji huo mapema kutokakana na mgonjwa kuwa na kiwango kidogo sana cha damu na hivyo kuendelea na kumpatia matibabu ya awali ikiwemo kumuongezea uniti tano za damu na ndipo wakaweza kumfanyia upasuaji

“Tulifanya vipimo kujiridhisha nini hasa chanzo cha uvimbe alionao, kwa muonekano wake uvimbe ulikuwa mkubwa kama mimba ya miezi tisa, baada ya vipimo tukafikia muafaka tumfanyie upasujai na hiyo ni baada ya kumuongezea damu kwa muda mrefu kwasababu alikuwa na kiwango kidogo cha damu cha g/dl 4 ambapo baada ya kufanya upasuaji ndipo tukafanikiwa kukuta uvimbe wenye kilogramu 6.4 kwenye kizazi (myoma) na kufanikiwa kuzitoa pamoja na kizazi”



Anasema kwa uzoefu wake kama Daktari bingwa wa magonjwa ya akina mama na uzazi Kilogramu 6.4 ni kiwango kikubwa cha uvimbe ambapo ameshauri akina mama kuwahi Hospitali wanapojihisi kuwa na matatizo yoyote kwenye uzazi au uvimbe tumboni

Zuwena aligundua kuwa ana uvimbe tumboni mwaka 2008 lakini alishindwa kupata matibabu kutokana na kushindwa kumudu gharama, kwasasa anaendelea na matibabu.